Uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050: Sekta ya Bima Yatajwa kuwa Nguzo Muhimu ya Ustawi wa Taifa

Uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050: Sekta ya Bima Yatajwa kuwa Nguzo Muhimu ya Ustawi wa Taifa

  • Date 17-07-2025

Dodoma, Juni 2025 – Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inalenga kuiwezesha nchi kufikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa misingi ya usawa, ubunifu, na ushindani wa kidijitali. Uzinduzi huo umefanyika jijini Dodoma, ukihudhuriwa na viongozi wa serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo. Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alieleza kuwa Dira ya 2050 ni mwongozo wa mabadiliko ya kina unaojikita katika kujenga taifa linalojitegemea, lenye uchumi wa viwanda, kijani na jumuishi, huku likitumia kikamilifu teknolojia ya kidijitali.

Miongoni mwa sekta zilizopewa kipaumbele kikubwa katika Dira hiyo ni sekta ya bima, ambayo imetajwa kama moja ya nguzo kuu katika kulinda ustawi wa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu.

Katika Dira ya 2050, serikali inalenga kuongeza matumizi ya bima kama njia ya kusimamia hatari katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, biashara, afya, miundombinu, na huduma za kijamii. Kwa mujibu wa Dira hiyo, lengo ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anakuwa na fursa ya kupata kinga dhidi ya majanga ya kifedha kwa kupitia huduma za bima.

“Tunatambua kuwa bima ni nyenzo ya kujenga uchumi imara na jamii yenye ustahimilivu. Dira ya 2050 inalenga kuongeza kiwango cha ushiriki wa wananchi katika huduma za bima kutoka chini ya asilimia 20 ya sasa hadi zaidi ya asilimia 70 ifikapo mwaka 2050,” alisema Waziri wa Fedha na Mipango, katika hotuba yake ya uzinduzi.