Wazazi wa Watoto sita waliopata ajali baada ya kugongwa na
gari aina ya Haice wakitokea kanisani, ambapo mmoja wao alifariki dunia,
wamekabidhiwa malipo ya gharama za matibabu na mazishi kutoka kwa kampuni ya
bima ya Bumaco Insurance.
Tukio hilo lililotokea mapema mwaka huu limeacha alama ya huzuni kwa jamii,
hasa kwa familia iliyompoteza mtoto wao.
Hata hivyo, kampuni hiyo ya bima imejitokeza kusaidia familia hizo kwa
kuzingatia masharti ya bima yaliyokuwepo kwa chombo kilichohusika katika ajali
hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi malipo hayo kwa wazazi wa watoto hao,
Meneja wa Mauzo wa Bumaco Insurance mkoa wa Kilimanjaro, Gasto Mrema,
amesisitiza umuhimu wa kuwa na bima, akisema ni kinga muhimu wakati wa majanga.
“Bima si anasa bali ni hitaji. Hakuna ajuaye kesho, hivyo ni vema kila mmiliki
wa chombo cha moto kuhakikisha anakata bima ili kusaidia wakati wa dharura kama
hizi,” alisema Mrema.
Hata hivyo amewashauri wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha kuwa
wanakata bima kwa ajili ya vyombo vyao ili kuwalinda wanapopatwa na majanga ya
ajali huku akiwasihi madereva kutokukubali kutembea na chombo cha moto
barabarani kisichokuwa na bima.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi wa watoto waliopata ajali hiyo wameishukuru
kampuni ya bima Bumaco Insurance kwa msaada waliopokea, wakisema umeleta faraja
katika kipindi kigumu walichopitia.
“Tumepitia maumivu makubwa, lakini msaada huu umetufuta machozi, tunawashukuru Bumaco
kwa moyo huu wa huruma, na tunatarajia waendelee kusaidia wengine watakapopatwa
na majanga kama haya,” alisema mmoja wa wazazi.
Ajali hiyo iliibua mjadala mpana kuhusu umuhimu wa bima za magari, huku wadau
wa usalama barabarani wakihimiza elimu zaidi kwa wananchi kuhusu sheria na haki
zao katika mifumo ya bima.